Kila Aprili Mosi ni siku ya upandaji miti kitaifa nchini Tanzania.Jeshi la zima moto Mkoani Morogoro leo limeshiriki katika kampeni hiyo iliyoandaliwa na Halmashauri ya Mji Ifakara ambayo imejipangia kupanda miti 10,000 katika kata zake 9 msimu wa masika mwaka huu.
Akizungumza mapema leo katika tukio la kupanda miti lililofanyika katika viunga vya Halmashauri ya mji Ifakara,Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Elia Shemtoi amelipongeza Jeshi la zima moto kwa kuungana na Watumishi wa Halmashauri katika tukio la upandaji miti na kuwashukuru kwa elimu ya kukabiliana na majanga ya moto ambayo jeshi hilo imeitoa mara baada ya zoezi la kupanda miti kukamilika.
"Kwakweli leo mmetufunza mengi,wengi wetu wamedhurika na kupoteza mali kwa kukosa elimu hii ya msingi tunawashukuru sana." Alisema Shemtoi
Naye Mkaguzi Msaidizi wa kikosi cha zima moto Hamadi Dadi aliyeongoza kutoa mafunzo hayo alisema Jeshi hilo lipo mbioni kufungua ofisi katika mji wa Ifakara kutokana na kasi ya ukuaji wa mji huo.
Akitoa maelekezo ya msingi kwa Watumishi kwa Watumishi wa Mji Ifakara ,Dadi alisema ni muhimu kuokoa maisha pale moto unapozidi kuliko kuokoa mali.Pamoja na kufundisha mbinu mbalimbali za kukabiliana na moto alisisitiza ujenzi unaozingatia tahadhari za majanga ya moto na kuongeza kuwa Jeshi la zima moto linafanya zaidi kazi ya kuzuia moto kwa kutoa elimu kwa Wananchi kwa 76% na 24% tu ndiyo kazi ya kukabiliana na moto pale unapotokea.
Nao Watumishi waliopata elimu hiyo walilishukuru Jeshi kwa kuwapatia elimu hiyo na kuliomba kuongeza kasi katika harakati za kuhamia mjini Ifakara huku wakitaka elimu ya kukabiliana na majanga ya moto kuelekezwa zaidi mashuleni kwa kuwa Wanafunzi wakielewa watapeleka ujumbe kwa Wazazi na hivyo sehemu kubwa ya Jamii itakuwa na uelewa wa kukabiliana na majanga hayo pindi yanapotokea.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa