Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa abiria na mizigo wa nchikavu na Majini ( SUMATRA) imesema ipo mbioni kuzikatia Leseni na kuzisajili Pikipiki zote za magurudumu matatu na mawili zinazotoa huduma ya kusafirisha abiria katika Mji wa Ifakara kwa Ushirikiano na Halmashauri ya Mji Ifakara na kwamba hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Usafirishaji na kanuni zake zilizoanza kutumika mwaka 2011.
Hayo yamethibitika katika kikao cha pamoja kati ya Wamiliki na Madereva wa Bodaboda na Pikipiki, SUMATRA na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama Barabarani wilaya ya Kilombero kilichoitishwa na Halmashauri ya Mji Ifakara kwa lengo la kuwapatia elimu Wamiliki na Madereva wa Vyombo hivyo vya usafiri kabla ya kuanza kwa zoezi la kuwasajili na kuwakatia Leseni hizo.
Afisa Mfawidhi wa SUMATRA Mkoa wa Morogoro ndugu Joseph Burongo ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria na kanuni ya Usafirishaji, Pikipiki zote za magurudumu matatu zinazotoa huduma ya kusafirisha abiria zinapaswa kusajiliwa na kupatiwa Leseni kwani Sheria hiyo na kanuni zake zilianza kutumika miaka saba iliyopita na kwamba SUMATRA imeingia makubaliano na Halmashauri zote nchini na kukasimu madaraka yake ya kuvikatia Leseni vyombo hivyo vya usafiri vinavyohudumia abiria kwa Halmashauri kupitia kitengo cha Biashara.
Afisa Mfawidhi huyo wa SUMATRA alifafanua kuwa kila chombo kinachotoa huduma ya kusafirisha abiria kina kiwango cha ada na leseni yake na kueleza kuwa kwa bodaboda ni Tsh.22,000/ wakati bajaji ni Tsh 32,000/ kwa mwaka mzima na kueleza kuwa ili mmiliki aweze kupatiwa Leseni hiyo atapaswa kufika Halmashauri ya Mji kitengo cha biashara, akiwa na nakala ya kadi ya chombo husika kwa wale ambao kadi hizo zimeandikwa majina yao na kwa wale ambao hawajahamisha umiliki watapaswa kuwasilisha nakala ya kadi iliyopo pamoja na nakala ya kitambulisho kimojawapo kati ya leseni ya udereva,kitambulisho cha Mpiga kura ,kitambulisho cha Uraia au Hati ya kusafiria na kwamba ada ya Leseni ya usafirishaji itaanza kutozwa katika kipindi husika cha usajili hata kama utekelezaji wa Sheria hiyo ulianza miaka saba iliyopita na kwamba hakutokuwa na Bajaji au Bodaboda itakayoruhusiwa kusafirisha abiria bila kuwa na Leseni ya Usafirishaji mara zoezi la usajili litakapoanza Ifakara.
Kwa upande wake Jeshi la Polisi kupitia kikosi cha Usalama barabarani wamewataka Waendesha Bodaboda hao kutii Sheria bila shuruti kwa kufuata Sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kusajili Vyombo vyao vya usafiri pamoja na vijiwe vyao kupitia Halmashauri kwa ajili ya kuwatambua Watoa huduma wote,kulinda usalama wao na usalama wa abiria wanaowaendesha
“Tunaachana na utamaduni wa kufanya kazi hii kwa mazoea na kuanza kuifanya kibiashara kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, ni kweli tumechelewa lakini ni lazima tufanye kwa mujibu wa Sheria ,mnapaswa kulinda Usalama wenu na abiria wenu ili shughuli hii iendelee kuwaingizia kipato bila bugudha.Sisi tunasimamia Sheria hivyo baada ya zoezi la usajili hakuna bajaji wala bodaboda itakayobeba abiria bila kuwa na Leseni ya usafirishaji.”Alisema Leus Yazidi Msimamizi wa nidhamu na Mtoa Elimu ya Barabarani Jeshi la Polisi Wilaya ya Kilombero.
Naye Kaimu Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kilombero Inspekta Nkilijiwa Lazaro, aliwataka Waendesha bajaji na bodaboda hao kuanza kujiandaa mapema ili kutii utaratibu huo mara usajili utakapotangazwa na Halmashauri kwani suala hilo ni la kisheria na hivyo halina mjadala na hata maeneo mengine utekelezaji wa Sheria hiyo umeanza muda mrefu na kuongeza kuwa angalau Watu wa Ifakara wamepata fursa ya kuelimishwa kabla ya kuanza utekelezaji, hivyo ni vyema wakatii maelekezo wanayopewa kwani utekelezaji wa Sheria hiyo ungeweza kuanza hata bila ya kutolewa Elimu kwa kuwa kutokujua Sheria sio kinga bali ni kosa pia.
Awali akifungua mkutano huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Francis Ndulane alisema kuwa wao kama Halmashauri ambao ndiyo wamekasimiwa madaraka ya utoaji wa Leseni hizo na SUMATRA wameona ni vyema kuwakutanisha Wadau wote na kuwapatia Elimu hiyo ili kuwa na uelewa wa pamoja ambao utarahisisha zoezi hilo ambalo litaanza hivi karibuni
Katika hatua nyingine Mkurugenzi Ndulane, aliahidi kusimamia Utaratibu wa kuunda Umoja wa Waendesha Bajaji na Pikipiki wote katika Mji wa Ifakara (TAMOSA) ili nao waweze kunufaika na fursa za mitaji zinazotolewa kupitia umoja huo na Wadau wa maendeleo ikiwemo mikopo ya fedha,pikipiki na bajaji na hatimaye Waendesha Bodaboda na Bajaji wa Ifakara waweze kumiliki biashara zao wao wenyewe, kuwa na vyanzo vya mapato zaidi ya kimoja, kukuza uchumi wa familia zao na kuchangia maendeleo ya Halmashauri ya Mji Ifakara na Taifa kwa ujumla.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa