WAZEE WATAKIWA KUENDELEA KUDUMISHA AMANI NCHINI
Wazee wa Halmashauri ya Mji Ifakara wametakiwa kuendelea kudumisha amani nchini haswa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu tarehe 29 Oktoba 2025 na kushiriki kutumia haki yao ya Msingi kwa kupiga Kura .
Rai hiyo imetolewa tarehe 1 Oktoba 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Wakili Dunstan Kyobya wakati alipokuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Kilama Kata ya Kibaoni, Halmashauri ya Mji Ifakara.
Aidha katika Maadhimisho hayo Mhe. Kyobya alisisitiza Jamii kuendelea kuwathamini Wazee na kuhakikisha wanapata haki zao za Msingi ikiwemo kupewa fursa ya kupata Mikopo ya Asilimia 10 na WBN.
“Maafisa Maendeleo ya Jamii hakikisheni Wazee wanapata Mikopo, umri wa Kijana umeongezeka kutoka Miaka 35 hadi 40 na kwa upande wa wanawake na watu wenye ulemavu umri hauna mwisho ili mradi ukidhi masharti ya Mikopo hiyo”. Alieleza Mhe. Kyobya.
Awali Wazee hao katika Risala yao walieleza Changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo changamoto za Afya, Migogoro ya Ardhi, Saikolojia, Sheria n.k
Wakati huo huo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Pilly Kitwana alisema kuwa Halmashauri imepokea changamoto za Wazee hao na kuahidi kuzifanyia kazi kwa haraka,baadhi ikiwemo changamoto za Bima ya Afya, Dawa n.k . Aidha alieleza kuwa baadhi ya Changamoto zimeshaanza kutatuliwa ikiwemo utoaji wa Kadi za Bima za Afya za CHF kwa wazee 300 na Wajane 300.
Aidha, takwimu zinaonesha Jumla ya Wazee Elfu 21, 468 wapo ndani ya Halmashauri ya Mji Ifakara kwa Kata zote 19 wakiwemo Wanaume 9611 na Wanawake 11857.
Kauli Mbiu katika Maadhimisho hayo kwa mwaka huu ilikuwa ni “Wazee Tushiriki Uchaguzi kwa Ustawi wa Jamii Yetu”.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa