Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Deodatus Philip Mwanyika (Mb), imefanya ziara yake katika Miradi mbalimbali inayopatikana Halmashauri ya Mji Ifakara, Wilayani Kilombero ambapo baadhi ya Miradi hiyo ni Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Tanzania (TARI) Ifakara, Ifakara White Rice Milling machines, pamoja na kiwanda cha Sukari Kilombero (K4) Februari 19, 2025.
TARI Ifakara kinajishughulisha na utafiti wa mazao mbalimbali, hususan mpunga, kwa lengo la kuboresha,uzalishaji na tija kwa wakulima pia kuweza kuja na mbegu bora zitakazo vumilia mafuriko.
Katika ziara hiyo, kamati imelenga kujionea shughuli za utafiti na maendeleo ya kilimo zinazofanywa katika kituo cha TARI Ifakara pia ilipata fursa ya kutembelea maabara za utafiti, shamba darasa, na maeneo mengine ya kituo, ambapo walijionea teknolojia na mbinu bunifu zinazotumika kuboresha kilimo.
Mhe. Mwanyika amezipongeza juhudi za TARI Ifakara katika kuendeleza sekta ya kilimo na kuhimiza ushirikiano zaidi kati ya kituo hicho na wadau mbalimbali ili kuhakikisha matokeo ya utafiti yanafikia wakulima kwa ufanisi na kuahidi kuja na namna bora ya kuongeza wafanyakazi ambao watakuwa wanawafikia wakulima moja Kwa moja.
Ziara hii inaendana na mikakati ya serikali ya kuinua sekta ya kilimo kupitia uwekezaji katika utafiti na maendeleo, ili kuongeza uzalishaji na kuinua kipato cha wakulima Halmashauri ya Mji Ifakara na nchini Kwa ujumla.
Mhe.David Silinde Naibu waziri wa Kilimo amesema wanaifakara wajifunze kuwekeza katika viwanda kwani serikali ipo tayari kuwaunga Mkono wananchi wote wenye nia ya kuwekeza kupitia Mfuko wa pembejeo (AGITF)ambao unajihusisha na utoaji wa Mikopo Kwa wakulima kwenye mnyororo wa kuongeza thamani.
Hata hivyo Kwa upande wake Mhe.Ng'wasi Kamani Mbunge Muwakilishi Vijana Taifa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imelenga kunyanyua watanzania wote kwani wamejionea uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa