Na: Nuru Mangalili - Ifakaratc , Habari
Vizimba Maalum kwaajili ya Kutupa Makopo ya Viuwatilifu vimetakiwa kujengwa katika kila Kata za Halmashauri ya Mji Ifakara ili kuweka udhibiti bora wa utunzaji wa taka ndani ya Halmashauri.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 5, 2025 na Afisa Tawala wa Wilaya ya Kilombero Bw. Fabius Byamungu aliyekuwa akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Wakili Dunstan Kyobya wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kihalmashauri iliadhimishwa kwa kufanya Usafi katika Soko Kuu la Ifakara lililopo Kata ya Ifakara.
Awali aliwataka Wananchi kuhakikisha wanakabiliana na changamoto za utunzaji wa Mazingira kwa kuwa kwa sasa Dunia imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira zinazotokana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ikiwemo utupaji hovyo wa taka ngumu na plastiki, ukataji holela wa miti na uchomaji wa misitu hivyo kusababisha madhara mbalimbali kama uwepo wa magonjwa hatarishi kama kansa kutokana na utupaji holela wa taka hatarishi kama chupa za viuwatilifu katika vyanzo vya maji na utumiaji wa chupa hizo majumbani kwa shughuli mbalimbali kama utunzaji wa mafuta ya kula, chumvi ,maji n.k uharibifu wa vyanzo vya Maji, ardhi kupoteza ubora na kupungua uwezo wa kuzalisha, upotevu wa viumbe hai wa ardhini na majini , ongezeko ya hali ya jangwa na ukame n.k.
Afisa Tarafa wa Ifakara Bw. Fabius Byamungu akizungumza na Wafanyabiashara wa Soko Kuu Ifakara juu ya Utunzaji wa Mazingira wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani
“Ili kukabiliana na changamoto za Utunzaji wa Mazingira na rasilimali wananchi wa Ifakara tunaowajibu wa kuhakikisha tunalinda na kutunza mazingira kwa kuzuia matumizi ya plastiki kuwa kibebeo cha bidhaa dukani, sokoni, buchani, n.k kuzuia utupaji hovyo wa makopo ya plastiki, ukataji miti hovyo na uvamizi wa maeneo ya hifadhi”. Alisema Bw. Byamungu na kuongeza “utupaji wa makopo ya viuwatilifu ufanyike kwenye vizimba maalumu ili kuweka utunzaji wa taka, hivyo kila Kata ijenge Kizimba maalum kwaajili ya kutupa makopo ya viuwatilifu. Alimaliza Bw. Byamungu
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Salome Mayenga aliwasisitiza Wananchi wa Ifakara kuhakikisha wanawajibika kutunza mazingira kwa kufanya usafi katika maeneo yao kila mara na kuepuka matumizi ya plastiki.
Kauli mbiu katika Maadhimisho hayo kwa Mwaka huu ni “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa , “ Dhibiti Matumizi ya Plastiki”.
****MWISHO*****
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa