KV-HELP YAGAWA KUKU 100 KWA WALENGWA WA KONGA ILI KUWABORESHEA LISHE NA KIPATO
Katika jitihada za kuboresha lishe na kipato kwa jamii watu wa ( KONGA)Wamekuwa wanufaika wa awamu ya kwanza kutoka Shirika la Kilombero Valley Health and Livelihood Promotion (KV-HELP) limegawa kuku 100 kwa walengwa 20 wanaohudhuria kliniki ya magonjwa sugu katika Halmashauri ya Mji Ifakara kupitia Mradi wa Health Chicken unaotekelezwa na Shirika la KV- HELP , Halmashauri ya Mji Ifakara na Chuo Kikuu cha Tiba cha Mtakatifu Francis ( SFUCHAS) ,ikiwa ni sehemu ya kuboresha maisha na lishe kwa walengwa hao.
Tukio hilo limefanyika tarehe 22 Septemba 2025 katika Ofisi za Shirika hilo lililopo Kapolo Ifakara.
Mgeni Rasmi katika tukio hilo alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara, Bw. Saidi Majaliwa, ambaye alipongeza hatua hiyo kama mfano bora wa ushirikiano kati ya serikali na taasisi zisizo za kiserikali katika kuinua maisha ya wananchi.
“Tunaishukuru KV-HELP kwa kuwa karibu na jamii, na kwa kuona mbali kwa kutoa msaada unaokwenda zaidi ya matibabu. Kuku hawa wanaweza kubadili maisha ya walengwa Hawa kwa kuwapatia lishe bora na fursa ya kujiongezea kipato,” alisema Bw. Majaliwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa KV-HELP, Bw. Iddy Mayumana, alisema kuwa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa shirika kusaidia walengwa wanaoishi na magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la damu, na VVU kwa njia endelevu.
“Watu wengi wanaoishi na magonjwa ya muda mrefu hukumbwa na changamoto ya lishe duni na hali ngumu ya kiuchumi. Tunatumia mbinu kama ufugaji wa kuku kuwasaidia kujenga uwezo wa kujitegemea,” alieleza Bw. Mayumana.
Walengwa waliopokea kuku hao walielezea furaha yao na kuahidi kutumia vizuri fursa hiyo. Wengi walisema kuwa msaada huo ni mwanzo wa kujikomboa kiuchumi na kuboresha afya zao kwa kula lishe bora inayopatikana kutoka kwa kuku, ikiwemo mayai na nyama.
Kwa mujibu wa KV-HELP, zoezi hilo ni sehemu ya mpango mpana wa shirika hilo wa kuimarisha afya na maisha ya watu walioko katika mazingira hatarishi kupitia miradi ya kijamii inayochangia afya na uchumi wa familia.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: -
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa