Wadau wa maendeleo wa Halmashauri ya Mji Ifakara wameboresha rasimu ya Mpango Mkakati wa miaka mitano wa kwanza tangu Halmashauri ilipoanzishwa Julai 2015 kwa kushiriki kutoa maoni ya mapendekezo yao katika kikao cha uwasilishaji wa rasimu hiyo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri.
Wakitoa mapendekezo yao baada ya kuwasilishiwa rasimu hiyo kisekta,Wadau hao wametaka Mpango huo kulinda rasilimali za misitu kwa kuonesha mikakati ya kupanda miti kibiashara, uwekezaji wa viwanda vya kuchakata magogo na mbao,Ulinzi shirikishi wa misitu kwa jamii, na kuwaelimisha Waganga wa Jadi kutochimba dawa katika misitu ya hifadhi.
Aidha katika kuboresha upatikanaji wa mapato wameitaka Halmashauri kuongeza mkakati wa kuanzisha stendi kubwa yenye ubora itakayokidhi mahitaji, kudhibiti upotevu wa mapato,kutenga maeneo maalum ya viwanda vya kuchakata Mpunga, kuandaa mpango shirikishi wa Jamii katika udhibiti wa uvuvi haramu,kuboresha na kuongeza mabwawa ya samaki kwa ajili ya kuongeza kipato kwa Wananchi kupitia ufugaji wa Samaki na kulinda rasilimali za mito na Kutoa elimu ya biashara kwa Wananchi ili kujihakikishia kipato chao na kuweza kulipa tozo za Serikali
Katika Sekta ya Elimu wametaka kuwepo kwa mkakati wa kuongeza shule,kukarabati zilizopo na kujenga Maktaba kwa ajili ya kuboresha mazingira ya elimu, huku katika sekta ya Afya wakitaka Wananchi kuhamasishwa kuanzisha ujenzi wa zahanati ngazi za vijiji na mitaa ili kupunguza msongamano wa Wagonjwa katika kituo cha Afya Kibaoni na katika Hospitali ya rufaa ya Mt.Fransisco, kuboresha dampo la takataka la Kiogosi kwa ajili ya kulinda Afya ya Jamii inayozunguka dampo hilo na kujenga miundombinu ya maji taka
Awali akiitambulisha rasimu ya Mpango Mkakati huo Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango, takwimu na Ufuatiliaji wa Halmashauri ya Mji ndugu Michael Danga, alisema Menejimenti iliandaa Rasimu hiyo kwa kila Sekta ikiwa ni hatua za awali za uundaji wa Mpango Mkakati kwa kuzingatia uwezo na udhaifu wa ndani wa Halmashauri pamoja na kufanya uchambuzi wa fursa na vikwazo ambavyo vipo nje ya Taasisi lakini hutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya Halmashauri.
Akifafanua kuhusu uwezo wa Halmashauri kwenye kutimiza majukumu yake Danga alisema kuwa Halmashauri ya Mji Ifakara inayo miundombinu yote muhimu ya kutolea huduma za kijamii kama vituo vya Afya,Maji na Elimu,uwepo wa Wataalamu wa fani mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji wa Sera za Serikali,kuratibu na kusimamia miradi ya maendeleo.Uwezo wa kukusanya mapato kwa rasilimali zilizopo,utulivu wa kisiasa,uwepo wa Sera,Miongozo na Sheria zinazosimamia utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri na uwepo wa Wadau wa Maendeleo na Wahisani .
Hata hivyo aliutaja udhaifu wa Halmashauri katika kutimiza majukumu yake kuwa ni pamoja na upungufu wa miundombinu ya kutolea huduma za kijamii,upungufu wa Watumishi,ukosefu wa soko la kisasa kwa ajili ya kuuzia bidhaa za kilimo na viwandani,ukosefu wa viwanda vya kisasa vya kuchakata mazao,uelewa mdogo wa Jamii katika masuala ya Ujasiriamali na kukuza Uchumi,ushiriki mdogo wa Wadau katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo na ukosefu wa jengo la Ofisi linalotosheleza mahitaji
Danga aliongeza kuwa Halmashauri inazo fursa za nje kama miundombinu ya barabara,reli ya TAZARA,umeme wa uhakika,Taasisi za kifedha,miundombinu ya mawasiliano ya simu,hali ya hewa nzuri,udongo wenye rutuba na mito yenye maji ya kutosha, ardhi kubwa kilimo na uwekezaji na kwamba Ifakara ni kitovu cha biashara kwa Wilaya na Mikoa inayoizunguka na kuzitaja baadhi ya changamoto kuwa ni ukosefu wa barabara ya kiwango cha Lami ,majanga ya asili kama mafuriko,uharibifu wa mazingira na ufinyu wa bajeti ya kutekeleza miradi ya maendeleo
Mchakato wa kupokea maoni ya Wadau ni hatua ya pili ya mwendelezo wa utengenezaji wa Mpango Mkakati huo kabla ya kuwasilishwa katika Baraza la Madiwani na Mamlaka za juu na ndipo utakapokuwa tayari kwa matumizi kuanzia mwaka 2018 - 2023 .
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa