Halmashauri ya Mji Ifakara imepokea vitabu 24,699 kutoka Shirika la misaada la Marekani USAID chini ya mradi wake wa ‘Tusome Pamoja’ unaojihusisha na kuwawezesha Wanafunzi wa shule za msingi hususani wa darasa la kwanza na la pili katika stadi tatu za kujua kusoma,kuandika na kuhesabu ambao unatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano.
Akizungumza wakati wa zoezi la kugawa vitabu hivyo kwa Walimu Wakuu wa shule za msingi 33 lililofanyika mapema leo katika viunga vya ofisi za Halmashauri ya Mji Ifakara Mkuu wa Idara ya Elimu Msingi Bi.Mariam Nnauye, amesema kuwa vitabu walivyopokea ni vya ziada kwa hatua ya kwanza hadi ya tatu katika kujifunza kwa darasa la kwanza na la pili na kwamba vitabu hivyo vina manufaa makubwa sana katika kuongeza stadi za kujifunza kwani huwavutia Wanafunzi kutokana na maudhui yaliyomo kuwafurahisha lakini pia vitabu hivyo ni vingi na vitaziba pengo la upungufu wa vitabu wa kiada kwa kutumika kama rejea katika Maktaba za Shule
Bi.Nnauye amesema kuwa upatikanaji wa vitabu hivyo ni matokeo ya tathmini ya utendaji mzuri wa Halmashauri ya Mji Ifakara katika miradi ya ‘UWAWA’ na ‘WAJE’ inayotekelezwa na USAID ambayo ililenga kuwajengea uelewa wa pamoja Wazazi,Walimu na Jamii kushiriki katika maendeleo ya elimu ikiwa ni pamoja na kuwapatia lishe Wanafunzi wakati wa masomo na kuongeza kuwa tathmini ya matokeo ya vitabu hivyo itafanyika baada ya kuanza kutumika na ikitoa matokeo mazuri Vitabu vya ziada vitaongezwa kwa Darasa la tatu na la nne
Kwa upande wao Walimu Wakuu wa shule za msingi waliopokea vitabu hivyo wamewapongeza na kuwashukuru Wadau hao wa elimu kwa kutoa vitabu hivyo na kueleza kuwa vitawasaidia sana kwani kuna upungufu mkubwa katika shule zao na kueleza kuwa watahakikisha vitabu hivyo vinatunzwa ili viweze kuwasaidia Wanafunzi wengi zaidi.
“Shule yangu ni miongoni mwa shule zenye upungufu mkubwa wa vitabu,binafsi nawashukuru sana ‘Tusome pamoja’ kwa kutupatia vitabu hivi kwani vitapunguza kwa kiasi kikubwa upungufu tuliokuwa nao.Tunawashukuru sana Wadau wetu na tunawaomba Wadau wengine kuendelea kuwekeza katika Elimu’.Alisema Mwalimu Victor Kabogwi wa Shule ya Msingi Mhola.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa