Mh. Mkuu wa wilaya ya Kilombero Ndugu James Ihunyo amewahimiza wasimamizi wa vituo vyote vya afya binafsi pamoja na taasisi za kidini kushiriki kikamilifu katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wote kwani hospitali, vituo vya afya na Zahanati za Serikali pekee haziwezi kukidhi kuwapatia mahitaji ya afya wananchi wote wa Ifakara Serikali kwa kulitambua hilo na kuona uhaba wa vituo hivyo vya kutolea huduma za afya, pia na wanajamii wengi wapo mbali na vituo vya Serikali vya kutolea huduma za afya, Serikali kwa nia njema ikaweka mpango mkakati kwa kushirikisha Sekta Binafsi, Taasisi za Kidini na watu binafsi zinazotoa huduma za afya ili ziweze kuwapatia huduma hizo za afya jamii.
Mkuu wa wilaya ya Kilombero ameyasema hayo wakati Halmashauri ya Mji Ifakara ikisaini mkataba wa makubaliano na Vituo viwili vya Afya (1. NESSA HEALTH CENTRE na 2. NIKO HEALTH CENTRE) pamoja na Zahanati moja (HAPPY DISPENSARY) kwa madhumuni ya vituo hivyo na Zahanati hiyo kuweza kuwapokea na kuwapatia huduma za afya wanachama wa chf iliyoboreshwa pale wanapokuwa na uhitaji wa huduma hizo. Aidha lengo kuu la kushirikisha vituo vya afya vya watu binafsi ni kuhitaji kuimarisha afya za jamii kwa kuweza kupata huduma za afya kwa wakati na kwa umbali mfupi kwa kutumia kadi za CHF ILIYOBORESHWA.
Hafla hiyo ya Kusaini mkataba wa makubaliano wa kutoa huduma za afya kwa wanachama wa CHF ILIYOBORESHWA ilifanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji kati ya Wakurugenzi wa vituo hivyo vya afya vinavyomilikiwa na watu binafsi na Zahanati inayomilikiwa na mtu binafsi vilivyopo ndani ya maeneo ya Mji wa Ifakara na Mheshimiwa wa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara pamoja Kaimu Mkurugenzi Mji Ifakara. Vituo vya kutolea huduma za Afya hivyo ni 1. NESSA HEALTH CENTRE, 2). NIKO HEALTH CENTRE na 3). HAPPY DISPENSARY. Aidha hafla hiyo fupi ilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya wa Kilombero, Mh. James Ihunyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilombero Ndugu Robert Selasela, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mh. Mashaka B. Mbilinyi, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mh. Chizza Shungu, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Ndugu Christopher Msimbe, Meneja CHF ILIYOBORESHWA Halmashauri ya Mji Ifakara Ndugu Mercy Gibson Minja, Mratibu wa CHF Mji ndugu Pilly Aziz, Wakurugenzi wa vituo hivyo, wadhamini wao na waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Mh. James Ihunyo amewapongeza na kuwashukuru wadau wa maendeleo wanaojishughulisha na utoaji wa huduma za afya kwa jamii kwa kuweza kuungana na serikali kuwa kitu kimoja katika utoaji huduma za afya kwa jamii. Alisisitiza kwa kusema kuwa wadau hawa wa huduma za afya wamekuwa mfano wa kuigwa katika mji wetu wa Ifakara. Alisisitiza kwa kufafanua kuwa tunategemea kuona wananchi wetu wakipatiwa huduma bora katika vituo vyenu vya kutolea huduma za afya na kuwatengenezea mazingira bora zaidi ya kupatiwa huduma hiyo kwa kutumia mfumo wa CHF ILIYOBORESHWA
"Aidha mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mheshimiwa Mashaka B Mbilinyi amefafanua kwa kusisistiza kuwa kwa kufanikisha kusaini mkataba wa makubaliano ya kutoa huduma za afya kwa wanachama wa CHF hii itasaidia sana kwa wananchi kuweza kufanya shughuli mbalimbali za kuwaingizia kipato kwa sababu watakuwa na afya bora na pale wanapokuwa na tatizo la kiafya atakuwa hana msongo wa mawazo kuwa atapata wapi pesa za kumsaidia kupata matibabu kwasababu atakuwa anayo kadi yake ya CHF ILIYOBORESHWA na ataitumia kwa mwaka mzima pale atakapokuwa na matatizo ya kiafya na anauhakika wa kupata huduma hiyo ya afya katika kituo kilicho karibu naye. Aidha aliongeza kuwa kwa kujiunga na kuwa mwanachama wa CHF ILIYOBORESHWA na kuingia mkataba na vituo hivyo vya kutolea huduma za afya itasaidia kutatua changamoto kama sio kuzimaliza kabisa, changamoto ya vifo vya wakinamama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Aliendelea kusisitiza kuwa Halmashauri itakuwa ikilipa kwa wakati madai yote yatayoletwa na vituo hivyo vya kutolea huduma baada ya kuwahudumia wanachama wa CHF ILIYOBORESHWA.''
Mmojawapo wa Wamiliki wa vituo hivyo vinavyotoa huduma za afya kwa jamii Dk Rashid Mayoka ambae ni Mkurugenzi wa Kituo cha afya cha NESSA ameahidi kuwa atahakikisha anawahudumia wananchi wote ambao ni wanachama wa CHF ILIYOBORESHWA na wengine wote kwa uweledi wa hali ya juu kama kiapo chao cha udaktari kinavyowaongoza. Aliendelea kufafanua kuwa ili kufikia Tanzania yenye viwanda tunahitaji kuwa na watu wenye afya bora kwani bila afya bora hatutaweza kufikia azma ya kuwa na Tanzania ya viwanda na hatimae kuwa na uchumi ulioimarika.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa