Halmashauri ya Mji Ifakara kwa Mara ya kwanza tangu kuanza kujitegemea mwaka mmoja uliopita imeshiriki Maonesho ya Kilimo,Uvuvi na Mifugo Kanda ya Mashariki yanayofanyika Mkoani Morogoro na kujumuisha mikoa ya Dar es Salaam,Pwani,Tanga na Morogoro
Akizungumza na Waandishi wa Habari katika eneo la mabanda na Vipando vya Halmashauri ya Mji Ifakara,Afisa Kilimo wa Halmashauri hiyo bibi.Happiness Mbele amesema Wakulima wategemee tofauti ya maonesho katika banda la Mji Ifakara kwa kujionea teknolojia na mbinu bora za uzalishaji wa mazao ya Kilimo na Mifugo unaofanyika kisasa na kupelekea uzalishaji wenye tija unaolenga Uchumi wa kati na Uchumi wa Viwanda
Afisa Kilimo huyo amesema miongoni mwa tofauti zinazopatikana katika banda la Mji Ifakara ni pamoja na bustani za kichanja,Mlima na kichuguu ambazo huhitaji eneo dogo lakini huzalisha kwa wingi na hutumia Maua maalum kuzuia Wadudu waharibifu wa mimea badala ya kutumia madawa yenye kemikali na hivyo kuhakikisha Afya ya Mlaji inabaki salama
Bibi Mbele amesema Teknolojia hiyo inawawezesha Wakazi wa Mjini wasio na maeneo makubwa na wanaoishi katika nyumba za kupanga kuweza kufanya Kilimo cha kujikimu na cha biashara hivyo kuongeza pato la familia hata bila kuwa na ardhi kwani aina hiyo ya Kilimo hufanyika hata katika vibaraza vya nyumba za kuishi na maghorofani
Naye Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri hiyo Bwana Elia Shemtoi amesema Idara yake imejipanga vyema kwani imeleta teknolojia za maonesho tofauti na yaliyozoeleka kama vile Ufugaji wa kuku juu ya Bwawa la Samaki ambapo teknolojia hiyo huchukua kipande kidogo cha ardhi lakini wakati huohuo kinyesi cha kuku hutumika kurutubishia chakula cha Samaki.
Shemtoi ameongeza kuwa teknolojia nyingine ya ufugaji iliyotofauti ni ile ya kutotolesha vifaranga vya Kuku kwa njia ya asili kwa kutumia mafuta ya tàa na boksi la mbao ambapo ameeleza kuwa teknolojia hiyo ni ya gharama nafuu lakini pia ni rahisi kwa matumizi ya ngazi ya familia.
Kwa Upande wake Afisa Habari wa Halmashauri hiyo bi. Fatna Mfalingundi ametoa wito kwa Wananchi wa kanda ya Mashariki kutembelea banda la Halmashauri ya Mji Ifakara kwenye maonesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Mwalim Julius Kambarage Nyerere Mkoani Morogoro na kueleza kuwa banda hilo linapatikana upande wa Mashariki ya uwanja njia ya kuelekea banda la VETA mita 100 kutoka Dar es Salaam 'Zoo' .
Bi Mfalingundi amesema kuwa Wakulima na watu wote wanaopenda Ujasiriamali na kukuza vipato vyao kwa mitaji nafuu ni vyema wakatembelea banda la Mji wa Ifakara kwani Halmashauri hiyo imedhamiria kuacha alama,kubadili mtazamo kuhusu Kilimo hasa kwa Wakazi waishio Mjini na kuleta athari chanya kwa Wakulima na Wajasiriamali wa kanda ya Mashariki kwa kuandaa maonesho hayo katika mtindo usio wa kawaida ' Business Unusual'
Afisa Habari huyo ameongeza kuwa pamoja na kujionea teknolojia za kipekee za kilimo na ufugaji Watembeleaji Watakaozuru banda hilo pia watapata burudani kemkem na kuona bidhaa za asili ya Mtanzania zilizotengezwa kwa ubunifu na ustadi wa hali ya juu kwa kutumia Mikono ya Wajasiriamali wa Ifakara.
Ameongeza kuwa mbali na Wajasiriamali wa kawaida Halmashauri yake haikuwaacha nyuma Wawekezaji Wakubwa kwani Ifakara ni Mji wa kimkakati katika Uwekezaji wa Viwanda na hivyo kuwaalika watu wote wanaotafuta fursa za uwekezaji wa Viwanda,Biashara na makazi kutembelea banda la Ifakara na kujionea fursa za kipekee zinazopatikana Ifakara
Maonesho ya Kilimo na Mifugo nanenane yamezinduliwa leo Agosti Mosi na Waziri wa Maliasili na Utalii Mh.Profesa.Jumanne Maghembe kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na yatafikia kilele chake Agosti 8, 2017.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa