MKURUGENZI HALMASHAURI YA MJI IFAKARA AKAGUA MWITIKIO WA WANAFUNZI KURIPOTI SHULENI
MKURUGENZI HALMASHAURI YA MJI IFAKARA AKAGUA MWITIKIO WA WANAFUNZI WALIORIPOTI SHULENI
Na: Nuru Mangalili - Ifakara Mji , Habari
Ikiwa ni siku ya kwanza ya kufungua Shule za Awali , Msingi na Sekondari Leo tarehe 13 Januari 2026 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bi. Pilly Kitwana amekagua hali ya wanafunzi kuripoti shuleni katika Shule Mbalimbali Zilizopo Halmashauri ya Mji Ifakara.
Akizungumza wakati alipokuwa katika Shule ya Sekondari Kilombero ,Bi. Pilly Kitwana aliwasisitiza Walimu kuhakikisha Suala la Lishe linatiliwa mkazo na kutoa Elimu ya kutosha kwa wazazi Ili wanafunzi wapatiwe Chakula Mashuleni na kuongeza Ufaulu .
Aidha Bi. Kitwana alitoa wito kwa Wazazi ambao bado hawajapeleka watoto Shuleni kuhakikisha watoto wanaripoti mapema Ili masomo yasiwapite.
" Shule zimefunguliwa leo ,hali ya wanafunzi kuripoti shuleni ni nzuri na wanafunzi wameanza masomo ,niwasihi wazazi wote ambao bado hawajapeleka watoto Shuleni wahakikishe watoto wameripoti shuleni bila kukosa". Alisema Bi. Pilly Kitwana na kuongeza" Walimu wote kwenye Shule zote za Halmashauri ya Mji Ifakara muhakikishe mnafundisha tangu siku ya kwanza wanafunzi wameripoti Shuleni. ". Alimaliza Bi. Pilly Kitwana
Kwa upande wake Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Ifakara Bwana Folkward Mchami alieleza kuwa Hali ya Wanafunzi kuripoti Shuleni ni kubwa na wanafunzi waliojiandikisha kidato cha Kwanza kwa shule zote imeongezeka na kuwasihi wazazi kuhakikisha watoto wote wanafika kuanza masomo kwa wakati.
Nae Afisa Elimu Msingi Bi. Witness Kimoleta alieleza kuwa wanafunzi walioripoti shuleni kwa siku ya Leo tarehe 13 Januari ni kubwa kuanzia Darasa la Awali Mpaka Elimu Msingi.