HALMASHAURI YA MJI IFAKARA YAENDELEA NA UTAMBUZI WA KAYA MASKINI
HALMASHAURI YA MJI IFAKARA YAENDELEA NA ZOEZI LA UTAMBUZI WA KAYA MASKINI
Na: Jacqueline Jerome - Ifakara TC, Habari
Mikutano ya wananchi imefanyika katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Mji Ifakara kwa lengo la kutambua na kuorodhesha Kaya zenye hali duni sana ambapo inajumuisha Kaya maskini pamoja na Kaya zilizo kwenye hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya hali ya hewa kama vile mafuriko na ukame ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuwatambua wananchi wanaohitaji msaada wa kijamii na kiuchumi.
Lengo la zoezi hili si kuandika majina ya kaya tu bali ni kusaidia Serikali iwe na taarifa sahihi zitakazoiwezesha kusaidia wananchi kwa haraka na kwa ufanisi pale kunapotokea dharura au wakati wa kutekeleza programu za kijamii.
Katika mikutano hiyo, viongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za mitaa na Kamati husika, waliwaeleza wananchi vigezo vinavyotumika katika utambuzi wa Kaya maskini ili kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa uwazi, haki na ushirikishwaji wa jamii, Miongoni mwa vigezo vilivyobainishwa ni pamoja na Kaya zenye kipato cha chini sana zisizo na uhakika wa kumudu mahitaji ya msingi ya maisha kama chakula, mavazi na makazi. Vigezo vingine ni Kaya zisizoweza kumudu au zisizo na uhakika wa kupata angalau milo kamili miwili kwa siku, Kaya zinazoishi katika makazi duni kutokana na kipato kidogo pamoja na Kaya zenye utegemezi mkubwa.
Aidha, Kaya zenye watoto wa umri wa kwenda shule lakini hawajaandikishwa shuleni au wameacha shule kutokana na kukosa mahitaji muhimu ya shule kama sare, madaftari na chakula nazo zimezingatiwa. Vilevile, Kaya zenye watoto wanaoshindwa kupata huduma za afya au kuhudhuria kliniki kwa kukosa uwezo wa kifedha, pamoja na Kaya zinazohudumia watoto wenye uhitaji maalum wa mahitaji muhimu kama makazi, mavazi, chakula, elimu na huduma za afya, zimeorodheshwa kama sehemu ya vigezo vya utambuzi.
Hata hivyo viongozi wa Halmashauri ya Kijiji /mtaa/shehia,kamati za jamii Viongozi wa dini waajiriwa,viongozi wa vyama,wastaafu wanaopokea pensheni hawaruhusiwi kuwa miongoni mwa kaya maskini.