KAMISHNA WA OPERESHENI NA MAFUNZO AKAGUA KITUO KIPYA CHA POLISI KIBAONI ,IFAKARA
KAMISHNA WA OPERESHENI NA MAFUNZO AKAGUA KITUO KIPYA CHA POLISI IFAKARA
Leo tarehe 12 Januari, 2026, Kamishna wa Polisi Idara ya Operesheni na Mafunzo, CP Awadhi Juma Haji, amefanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kilombero, Mkoani Morogoro, ambapo amekagua Maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kipya cha Polisi Ifakara.
Katika ziara hiyo, CP Awadhi Juma Haji ameipongeza Kamati ya Ujenzi kwa usimamizi mzuri wa Mradi huo muhimu, akieleza kuridhishwa na kasi pamoja na ubora wa ujenzi unaoendelea ambapo hadi sasa ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 99, hatua inayoashiria kukaribia kukamilika kwake.
Aidha Kamishna huyo amewataka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama pamoja na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilombero SSP Daud Nkuba kuhakikisha kuwa usalama wa jengo hilo jipya vinaimarishwa wakati wote, kutokana na kuwa ujenzi bado unaendelea na jengo likiwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.
Akihitimisha ziara yake, CP Awadhi Juma Haji amemshukuru Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro pamoja na uongozi wa Polisi Wilaya ya Kilombero kwa mapokezi mazuri, ushirikiano na maandalizi yaliyowezesha ziara hiyo kufanyika kwa mafanikio