Jukwaa la Wanawake wa Halmashauri ya Mji Ifakara lililozinduliwa hivi karibuni na katibu Tawala wilaya ya Kilombero kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, linatarajiwa kuleta mabadiliko chanya na kuondoa ombwe la uchumi kati ya Wanaume na Wanawake wa Mji wa Ifakara na hivyo kupunguza unyanyasaji unaofanywa na baadhi ya Wanaume kwa Wanawake.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa dawati la uwezeshaji Wananchi kiuchumi wa Halmashauri hiyo bibi.Ester Mtweve alipozungumza na Waandishi wa habari baada ya Uzinduzi wa Jukwaa hilo la kwanza Mkoani Morogoro tangu kutolewa kwa agizo la kuundwa kwa Majukwaa hayo.
Mtweve amesema kuwa kwa miaka mingi wanawake wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogondogo ambazo haziwapeleki kwenye uchumi mkubwa tofauti na Wanaume ambao wamekuwa wakijishughulisha kwenye uwekezaji mkubwa, hivyo kuelekea Tanzania ya Viwanda jukwaa hilo lina lengo la kuwaunganisha Wanawake katika chombo kimoja na kuwapatia elimu pamoja na fursa katika uwekezaji mkubwa hasa kwa kuwa muundo wa jukwaa hilo unahusisha wajumbe toka Serkalini, Sektabinafsi, asasi za kiraia, asasi za kijamii, asasi za kidini, Wadau wa maendeleo ,taasisi za fedha, Wahisani pamoja na Wanawake wanajamii wa kawaida.
“Jukwaa hili ni sauti ya pamoja ya wanawake kwa kuwa fursa zilizopo kwa Wadau wa Maendeleo zikiwemo NGO na Wahisani zitaunganishwa moja kwa moja kwa Wanawake wanajamii wa kawaida ambao nao watakuwa wamewasilisha mahitaji yao ya mitaji baaada ya kupatiwa elimu kupitia majukwaa ya mitaa,vijijina kata.”AlisemaMtweve.
Mtweve aliongeza kuwa jukwaa hilo lina kazi ya kuwaunganisha Wanawake na Taasisi zinazoshughulika na ubora wa uzalishaji wa bidhaa kama SIDO,BRELA,Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuhakikisha bidhaa zitakazozalishwa na Wanawake walio katika Jukwaa hilo zina ubora sambamba na kuwapatia namba za utambulisho wa bidhaa (barcode) na hivyo kuwawezesha kufanya biashara kimataifa, hivyo amewataka Wanawake kuendelea kujiunga katika vikundi ili fursa zinapokujazikiwemo Tsh. 50,000,000/- zilizoahidiwa na Viongozi wa kitaifa wawe wameshajiandaa.
Awali akizindua Jukwaa hilo, Katibu Tawala wilaya ya Kilombero ndugu Robert Selasela aliitaka Halmashauri kusimamia uundwaji wa majukwaa hayo katika kata zake zote ifikapo Juni 30 mwaka huu, kuwapatia elimu ya Ujasiriamali na upatikanaji wa mitaji, sambamba na kuwaboreshea mazingira ya biashara kwani Wanawake ndiyo walezi wa familia.
Kadhalika baada ya Uzinduzi wa Jukwaa hilo Wanawake zaidi ya 300 waliohudhuria uzinduzi huo walifanikiwa kufanya uchaguzi wa viongozi wao utakaodumu kwa miaka 3 ambapo nafasi ya Mwenyekiti wa Jukwaa hilo imechukuliwa na Dkt. lrene Kasiga kutoka hospitali ya Mt. Francis, Makamu Mwenyekiti ni Christina Livangala (Mjasiriamali),Katibuni Mercy Minja (Afisa Maendeleo ya Jamii Mji) na nafasi ya Mweka Hazina ikichukuliwa na Elizaberth Wapalilawa (Yetu Microfinance Benki).
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa