Wananchi na Wadau wa usafirishaji katika Halmashauri ya Mji Ifakara wameunga mkono jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo kwa kukubali kuwa wapo tayari kuhamia stendi kuu ya Kibaoni kutoka ile ya ‘Kwamakali’ na kukiri kuwa stendi hiyo inayotumika sasa ni ndogo,ina mazingira duni ya kufanyia kazi zao na ipo katikati ya makazi ya watu
Wakizungumza na Waandishi wa habari waliofika katika stendi ya Kwamakali kujionea hali halisi ya stendi hiyo Wananchi hao wamesema wanatambua nia nzuri ya Serikali na kueleza kuwa katika nchi hii Miji mingi hutanuliwa kwa mtindo kama huo wa kusambaza huduma za kijamii katika maeneo ya pembezoni, hata hivyo waliishauri Halmashauri kuiimarisha stendi ya Kibaoni kwa kuweka huduma muhimu kama choo,banda la kupumzikia abiria na taa kwa ajili ya ulinzi wa mali zao na ndipo waweze kuhamishiwa katika stendi hiyo mpya yenye eneo kubwa na inayokidhi idadi ya magari yanayoingia Ifakara kwa sasa .
“Kweli eneo hili tulilopo sasa ni dogo,kwanza ni chafu na halina mazingira bora ,kipindi cha masika tunapata tabu sana na kwa sasa stendi hii haitoshi kulingana na wingi wa magari yaliyopo,tunakubaliana na Serikali kuhamia stendi ya Kibaoni lakini mazingira ya Kibaoni yaboreshwe kama tulivyoomba”Alisema Mohammedi Ramadhani Wakala wa Usafirishaji katika stendi hiyo.
Naye Allan Ngomahela Mfanyabiashara ya usafiri wa bodaboda amesema kuhamishwa kwa stendi hiyo ni sahihi kabisa na ni fursa nzuri kwa Wafanyabiashara wote wakiwemo ‘mama ntilie’ na wengine kwani kutakutakuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na hivyo watatanua biashara zao na kuongeza vipato na kueleza kuwa kwa upande wa bodaboda na bajaji wataongeza pato lao kwa sababu abiria wanaotoka Mahenge,Malinyi na Mlimba stendi yao itaendelea kuwa Kwamakali na hivyo itawabidi kuwabeba abiria wanaotaka kuelekea Morogoro na mikoa mingine kuwapeleka Stendi ya Kibaoni,lakini pia watalazimika kuwabeba abiria wanaotoka Morogoro na mikoa mingine na kuhitaji kwenda wilaya za Mahenge na Malinyi kuwapeleka katika stendi ya Kwamakali ili waweze kupata gari za maeneo hayo.
“Miji hutanuka kwa dizaini hiyo,Morogoro stendi ilihama na biashara zilitanuka mji unaendelea kukua,kuhama stendi sio tatizo bali Serikali iboreshe zaidi mazingira ya stendi mpya”.Alisisitiza Ngomahela
Hata hivyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Ndugu Christopher Msimbe aliyeambatana na Waandishi wa habari, alieleza kuwa Halmashauri ina mipango mizuri kuhusu stendi mpya na kusema kuwa walishakaa kikao cha pamoja na Wadau hao wa usafirishaji ambapo kwa pamoja walijadili changamoto zilizopo katika stendi mpya na tayari Halmashauri imeanza kuzifanyia kazi ambapo banda la kupumzikia abiria limekwishaanza kujengwa na taa za ulinzi zitawekwa likishakamilika.
Aidha aliongeza kuwa, Mkandarasi wa kujenga choo amekwishapatikana na amepewa muda wa wiki mbili kuwa ameshakamilisha ujenzi huo na tayari watu walionunua maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vibanda vya biashara katika stendi hiyo wote wamekwishaoneshwa maeneo yao kwa ajili ya kuendelea na ujenzi.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa