Shirika lisilo la kiserikali la Light for the World kutoka nchini Ubelgiji kwa kushirikiana na hospitali ya rufaa ya Mt.Francisco wanatarajia kupima macho wanafunzi 26,447 kutoka shule za msingi katika Halmashauri ya Mji Ifakara na watakaobainika na matatizo ya macho watatibiwa bure.
Zoezi hilo ni utekelezaji wa mpango wa miaka mitatu wa huduma za upasuaji na matibabu ya macho kwa wanafunzi wa shule za msingi za Halmashauri tatu katika mkoa wa Morogoro ambazo ni Mji Wa Ifakara na Halmashauri za wilaya ya Kilombero na Malinyi.
Akizungumza, katika uzinduzi Wa Mpango huo uliofanyika katika shule ya msingi Kikwawila,Kiongozi Wa mradi huo ambaye pia ni daktari bingwa Wa macho toka hospitali ya Mt.Francisco Dk Aza Lyimo, amesema Mpango huo utahusisha watoto wa kuanzia darasa la kwanza hadi la tatu katika shule zote za Halmashauri ya Mji Ifakara na huduma hiyo ya upimaji na matibabu itatolewa bure katika hospitali ya rufaa ya Mt.Francisco.
Dk Lyimo amesema Mpango huo ulianza kwa majaribio katika shule 8 mwaka Jana na waligundua kuwa asilimia 10 ya watoto waliopimwa kukutwa na matatizo ya macho yanayohitaji tiba na changamoto waliyobaini ni wazazi Wa watoto hao kukosa uwezo Wa kuwatibia watoto wao.
Amesema baada ya kubaini hilo walitafuta wafadhili na kuwapata shirika la Light for the World ambao watagharamia matibabu ya macho kwa watoto wote wataopatikani na matatizo ya macho ikiwemo vipimo,miwani na hata upasuaji na lengo ni kusaidia watoto hao wenye uono hafifu waweze kuona na kufanya vizuri katika masomo yao.
Akizindua Mpango huo,Mkuu Wa Wilaya ya Kilombero ndugu James Ihunyo amewashukuru wafadhili hao kwa kuhudumia shule 133 katika Wilaya ya Kilombero na kuwahakikishia kwamba maeneo yote wataalamu watakayotembelea watapokelewa vizuri na kupima wanafunzi wote.
Ihunyo amesema kupimwa kwa watoto hao na kupatiwa matibabu kutasaidia kupunguza gharama kwa wazazi na kutoa wito kwa wakurugenzi na maafisa elimu kushirikiana na wataalamu hao ili kumaliza tatizo la macho kwa wanafunzi wilayani humo.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi katika Halmashauri ya Mji Ifakara bi Mariam Nnauye amesema huduma hiyo itafika katika Shule za Msingi 40 zikiwemo 33 za serikali na 7 za watu binafsi na wanafunzi 26,447 watapata huduma hiyo na kusema kuwa kabla ya kuanza kwa Mpango huo walikuwa na kitengo kimoja cha upimaji Wa macho katika shule ya msingi Lumemo ila sasa Mpango huo utasaidia katika Halmashauri nzima.
|
|
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa