Kamati ya kudumu ya Fedha na Utawala ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Ifakara imefanya ziara ya kawaida ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ikiwa ni robo ya kwanza katika mwaka wa Fedha 2017/2018 na kuridhishwa na hatua zilizofikiwa kwa miradi mipya iliyoanzishwa na Halmashauri ikiwemo ujenzi wa machinjio ya Nguruwe iliyopo Kata ya Katindiuka, ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Mahutanga katika Kata ya Lumemo ,ujenzi wa shule tanzu ya Makero iliyopo kata ya Michenga na ujenzi wa Maabara katika shule ya sekondari ya Kilombero.
Wakiwa katika mradi wa Machinjio Katindiuka Wajumbe wa Kamati hiyo walifurahishwa na kasi ya ujenzi wa Machinjio hiyo iliyoanza kujengwa Julai mwaka huu ambapo inatarajiwa mara baada ya kukamilika kwake Machijio iliyopo katika Kata ya Mlabani itahamishia shughuli zake katika Machinjio hiyo ya kisasa ya Katindiuka.
“Mradi huu una ubora wa hali ya juu kabisa tunatarajia utaongeza mapato ya Halmashauri na kuzalisha Ajira ikiwa tutauwekea mazingira mazuri ya ufanyaji kazi wake ikiwemo matengenezo ya barabara”. Alisema Mh.Mashaka Mbilinyi Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Katindiuka alisema wao kama kata wamejipanga kuhakikisha mradi huo unafanya kazi vizuri kwani tayari wameshauwekea mpango wa kupata kisima kimoja kati ya Visima 10 vitakavyochimbwa kwa ushirikianao kati ya Halmashauri na Taasisi ya Marekani ya ‘Help Underserved Community (HUC)’
Katika hatua nyingine akizungumza na Uongozi wa Kisima cha maji katika Kata ya Mbasa kilichokarabatiwa kwa fedha za mfuko wa jimbo, Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mh.Mashaka Mbilinyi aliutaka uongozi huo kuweka utaratibu wa kukusanya fedha kwa Watumia maji wote wa kisima hicho na kuzihifadhi kwa ajili ya ukarabati wa kisima pindi kinapoharibika.
Kadhalika Kamati hiyo pia imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa shule tanzu ya Makero ‘Satelite School’ inayojengwa katika kijiji cha Michenga ambayo ilianzishwa kwa nguvu za Wananchi kwa lengo la kuwaondolea Wanafunzi wa shule ya Msingi adha ya mwendo mrefu ambapo awali walilazimika kutembea umbali wa kilomita 5 kuifuata shule ya kijiji.Tayari shule hiyo imekwishaanza kutumika baada ya Halmashauri kuridhika na matokeo ya nguvu za Wananchi na hivyo kupeleka fedha za Mfuko wa Jimbo pamoja na mradi wa P4R kwa ajili ya kuendeleza Ujenzi wa shule hiyo yenye vyumba viwili vya madarasa,ofisi pamoja na matundu 6 ya Choo.
Pamoja na miradi hiyo Kamati pia ilikagua maendeleo ya uboreshaji wa stendi kuu tarajiwa ya Kibaoni,umaliziaji wa nyumba ya Mwalimu shule ya sekondari Kiyongwile,zahanati ya kijiji Mahutanga na ujenzi wa madarasa 3 na choo wa shule tanzu ya Kiogosi inayolenga kuwaondolea adha ya mwendo mrefu Wanafunzi wa shule ya Msingi Ihanga iliyopo kata ya Lumemo na kuhimiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili kuweza kukidhi lengo lililokusudiwa
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa