Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Francis Ndulane amewahimiza vijana kushiriki michezo na kufanya mazoezi ya viungo kuwa ni utamaduni wao wa maisha ili kuweza kukabiliana na hisia zinazoweza kuwashawishi kufanya vitendo hatarishi vinavyoweza kupelekea kupata maambukizi ya UKIMWI.
Mkurugenzi ameyasema hayo katika bonanza la michezo lilifanyika katika viwanja vya Bethlehem ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani na kuwashirikisha Watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara,Wilaya Kilombero na Watangazaji wa redio Pambazuko
“ Leo tumecheza kwa pamoja kwa ajili ya kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani na kuongeza hamasa ya michezo hivyo ni vyema utamaduni huu tukaundeleza ili kuchangia kupunguza maaambukizi ya UKIMWI kwani watu wakitoka kwenye michezo huwa wamechoka na hivyo kuwaondolea fikra za mambo yanayoshawishi vitendo hatarishi.”Alisema Ndulane
Kadhalika Mkurugenzi aliwasihi Vijana na Watu wote waliojitokeza kushiriki bonanza hilo kujiwekea utaratibu wa kupima Afya zao mara kwa mara na kueleza kuwa katika siku hiyo zaidi ya watu 100 akiwemo yeye mwenyewe walipima kwa hiyari Virusi vya UKIMWI mapema siku hiyo katika maadhimisho yaliyotangulia kufanyika kwenye Viwanja vya shule ya Msingi Lipangalala
Aidha Ndulane alieleza kuwa kasi ya Maambukizi ya UKIMWI katika Halmashauri ya Mji Ifakara imepungua kutoka 6.7% ya mwaka jana hadi 5.3% na kusema kuwa hata hivyo kiwango hicho bado ni kikubwa na kuwataka watu wote kuendelea kujilinda kutopata maambukizi na hasa ikizingatiwa kuwa Ifakara ni Mji wa biashara na hivyo una mwingiliano mkubwa wa watu
Katika bonanza hilo lililohusisha mchezo wa mpira wa miguu kwa Wanaume,netiboli na kuvuta kamba baina ya timu ya Bomani iliyowajumuisha Watumishi wa Halmashauri za Mji Ifakara na Wilaya ya Kilombero baina ya Watangazaji wa redio Pambazuko, timu ya Watumishi wa Bomani iliibuka kidedea katika michezo yote mitatu ambapo katika Netiboli iliifunga timu ya redio Pambazuko magoli 16 kwa 11 na katika mpira wa miguu Bomani ilishinda kwa penati moja dhidi ya Pambazuko.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa