Katika kuendelea kuimarisha Utawala bora Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Ndugu Francis Ndulane ameketi katika kikao cha pamoja na Wenyeviti wa Vijiji na vitongoji vyote vya Halmashauri ya Mji kujadili mustakabali wa nafasi na maslahi ya wenyeviti hao sambamba na kuzumngumzia maendeleo ya Mji Ifakara kwa ujumla.
Akiwakaribisha katika kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki Ndulane aliwapongeza Wenyeviti hao kwa kujitokeza kwa wingi na kuhudhuria kikao hicho na kuwaomba uhudhiriaji huo pia uwe wenye ufanisi katika Mikutano ya baraza ambayo hualikwa ili kuweza kupata majibu ya moja kwa moja yanayohusu maeneo yao na kupeleka mrejesho kwa Wananchi wanaowaongoza.
Ndulane alisema kuwa kwa mujibu wa muongozo alioupokea hivi karibuni unaelekeza Wenyeviti wa mitaa 33 kuendelea kutambulika kama Wenyeviti wa Vitongoji hadi pale Uchaguzi wa wenyeviti wa Mitaa utakapofanyika kwani uchaguzi uliofanyika mwaka 2014 katika mitaa hiyo 33 walichaguliwa Wenyeviti wa Vitongoji badala ya Mitaa.
Mkurugenzi amewasihi Wenyeviti hao kuwa wavumilivu na kuendelea kuzitumikia nafasi hizo kwa moyo hadi pale uchaguzi mwingine utakapofanyika na kuwaeleza kuwa ikiwa hali ya uchumi wa halmashauri itakuwa nzuri uchaguzi huo unaweza kufanyika mwakani kwa mitaa yote kwani kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali Halmashauri za Miji huwa na Wenyeviti wa Mitaa,lakini ikishindikana itawalazimu kusubiri uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 hasa kwa kuwa Halmashauri bado ni changa na hivyo fedha nyingi zinaelekezwa katika uimarishaji wa miundombinu na huduma kwa jamii na hata ongezeko la posho zao wataanza kulipwa katika mwaka mpya wa fedha wa Serikali Julai 2017.
Nao Wenyeviti hao walioafikiana na muongozo huo waliomba ongezeko la posho zao kuanza kulipwa kwa wakati na kumshauri Mkurugenzi kuongeza nguvu katika ukusanyaji wa mapato kwa kupanua wigo wa mapato ikiwemo mapato ya ardhi kwa kupima viwanja vingi na maeneo ya wakazi,kuanza matumizi ya stendi ya Kibaoni na kuboresha miundombinu ya stendi Makali ili kuongeza mapato
Awali akifungua Mkutano huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Viwanja 60 ‘B’ Mh.Mashaka Mbilinyi alisema kikao hicho kimetokana na msukumo wa changamoto ya utendaji kazi wa Wenyeviti hao ambao ulisababishwa na baadhi yao kupandishwa hadhi na kuwa Wenyeviti wa Mitaa huku wakiendelea kutumia mihuri ya Wenyeviti wa Vitongoji jambo lililopekea kuomba maelekezo ambayo hatimaye yametolewa na Muongozo uliowasilishwa.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa