Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Elia Shemtoi amewataka Wananchi wote hususani waishio maeneo hatarishi ya mabondeni kuhama katika maeneo hayo kwa ajili ya usalama wao na mali zao kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ikiwa ni hatua ya tahadhari dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mafuriko.
Shemtoi amesisitiza kuwa Wahanga walioathiriwa na mvua hizo mwaka jana ambao bado wameendelea kuishi katika maeneo hayo wanatakiwa kuondoka haraka kwani mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimekwishaanza kuleta madhara katika maeneo hayo.
Ameyataja maeneo yaliyoathiriwa mwaka jana kuwa ni Kata ya Lumemo hususani Wakazi waishio pembezoni mwa bonde maarufu kwa jina la Karolina na kuongeza kuwa maeneo mengine yaliyoko hatarini ni pamoja na Kiyonjo,Lihami ,Upogoro,Igombati na Lumemo ‘A’ na ‘B’
Aidha Kaimu Mkurugenzi pia amezitaka Serikali za Mitaa na Vijiji kushirikiana na Jamii husika kuweka alama katika maeneo ya makazi ambayo ni hatarishi kutokana na mashimo yaliyochimbwa kwa shughuli mbalimbali kwakuwa kwa sasa hayaonekani kutokana na kufunikwa na maji.
Kadhalika amewataka Wazazi na Walezi kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki cha mvua za masika kutokana na mashimo na mito kujaa maji kupindukia.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa