Hospitali ya rufaa ya Mt.Francis imesaini mkataba na Halmashauri ya Mji Ifakara wa Kutibu Wagonjwa wanaotumia kadi za Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) iliyoboreshwa sambamba na kuanzisha dirisha maalum la Wazee ikiwa ni hatua ya kutanua wigo wa upatikanaji huduma za matibabu kwa Wanachama wa CHF.
Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Francis Ndulane katika mkutano wake na Vyombo vya Habari uliofanyika ofisini kwake na kuhudhuriwa na Wawakilishi wa redio za Ulanga FM, Pambazuko FM na Aboud Media.
Mkurugenzi ameeleza kuwa ikiwa inaelekea kutimia miaka miwili tangu Halmashauri ya Mji ianze kujitegemea kazi kubwa ya kuboresha huduma za Afya imefanyika kwa kuboresha kituo cha Afya Kibaoni ambapo sasa huduma ya ‘X-ray’ inatolewa kituoni hapo na tayari Wadi mpya 5 zimefunguliwa na kufanya kituo hicho kuwa na uwezo wa kulaza Wagonjwa 128 kwa pamoja ambapo huo ni sawa na uwezo wa Hospitali.
Aidha ameongeza kuwa gari la Wagonjwa wa dharura ‘Ambulance’ iliyokuwa katika matengenezo makubwa imekwishatengemaa na hivi karibuni imeanza kutoa huduma katika kituo hicho ambapo sasa adha ya Wajawazito na Wagonjwa Mahututi waliokuwa wakisafirishwa kwa Bajaji kupelekwa katika Hospitali ya rufaa ya Mt.Fransis imekwisha na kuongeza kuwa mpango wa kununua ‘ambulance’ mpya kwa mapato ya ndani mwaka huu wa fedha unaendelea ambapo jumla ya shilingi bilioni 2.2 zinatarajiwa kukusanywa na bilioni 1.9 sawa na 60% zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ununuzi wa ambulance na gari moja la kawaida.
Kadhalika Mkurugenzi Ndulane amesema kuwa Halmashauri inaendelea kufanya mazungumzo na Zahanati za Misheni za Kikwawila na Viwanja Sitini ili nazo ziweze kupokea Wanachama wa CHF na kupunguza msongamano katika kituo cha Afya Kibaoni na Hospitali ya rufaa ya Mt.Francis wakati mpango wa uhamasishaji wa jamii kuanza ujenzi wa Zahanati katika mitaa na vijiji vyao ukiendelea na kueleza kuwa tayari baadhi ya maeneo wameitikia wito huo na kukitaja kijiji cha Mahutanga kuwa tayari wamenyanyua boma na Kata ya Viwanja sitini wameanza kuhamasishana kuchangia na kwamba wote hao wataongezewa nguvu ya kifedha na Serikali pindi wakifikia hatua ya kupaua.
Ndulane amewapongeza Wananchi waliojiunga na CHF na kuwasihi ambao bado kuendelea kujiunga kwani dawa katika Hospitali za Mji wa Ifakara zinapatikana kwa 95% huku kiwango cha kujiunga kikiwa ni Tsh 10,000/- kwa kaya ya watu 6 ambapo wataweza kupata huduma za Afya katika zahanati ya Michenga,kituo cha Afya Kibaoni, Hospitali ya rufaa ya Mt.Fransisco na baadae katika zahanati za Misheni za Kikwawila na Viwanja sitini pindi taratibu za mikataba zikishakamilika.
Hata hivyo Mkurugenzi ameeleza kuwa Halmashauri imefanya mabadiliko kwa kumuondoa aliyekuwa Meneja wa CHF na sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Afisa Maendeleo ya Jamii, Bibi.Mercy Minja ambaye katika muda wa miezi mitatu amefanya kazi kubwa ya kuongeza idadi ya Wanachama wa CHF kutoka 6% iliyokuwepo mpaka 11.05% ya sasa.
Kadhalika Ndulane amewasihi Wananchi kuendelea kulipa Ushuru na kodi mbalimbali za Serikali kwani kupitia fedha hizo ndipo Halmashauri itaweza kuboresha miundombinu ya huduma za kijamii ikiwepo ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia mzunguko wa Kibaoni hadi TAZARA yenye urefu wa kilomita mbili.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa