Benki ya NMB Tawi la Ifakara imeadhimisha wiki ya huduma kwa Wateja kwa kufanya Majadiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara kwa lengo la kubaini mafanikio na changamoto za utoaji huduma wa Benki hiyo kwa Halmashauri ya Mji ambao ni Wadau wakubwa wa huduma za NMB.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika mapema leo asubuhi kwenye ukumbi wa NMB, Meneja wa Tawi la NMB Ifakara ndugu Abdallah Chakachaka, amesema kuwa ni utamaduni wa Benki ya NMB kuadhimisha wiki ya huduma kwa Wateja kwa kuzungumza na Wateja na kupokea maoni yao, na kwamba wanafurahia Ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kutoka Halmashauri ya Mji Ifakara ambapo Ushirikiano huo umekuwa chachu ya uboreshaji wa huduma za NMB na kufikia Oktoba 15 Mwaka huu Benki hiyo itafungua Mashine ya ‘ATM’ karibu na Ofisi kuu ya Halmashauri ya Mji ili kusogeza huduma karibu na Wadau wao.
Meneja Chakachaka ameongeza kuwa benki yake imeanzisha fursa nyingine ya mkopo maalum kwa Watumishi ujulikanao kama “Motgage Finance”ambao utawawezesha Watumishi kuchukua kiasi kikubwa cha fedha na kulipa kwa muda mrefu zaidi ya miaka 10 na una riba nafuu kulinganisha na mikopo mingine na kubainisha kuwa ili kuendelea kutoa huduma bora na kupunguza mzigo kwa Tawi la Ifakara , NMB itaanzisha Matawi mawili maeneo ya Malinyi na Mlimba kufikia mwaka 2018.
Kwa upande wake Meneja huduma kwa Wateja wa NMB ndugu Asha Mlawa amemuomba Mkurugenzi kufikisha salam za NMB kwa Watumishi wa Halmashauri ya Mji Ifakara na kuongeza kuwa wao NMB wanajisikia fahari kuihudumia Halmashauri ya Mji kwani imekua ikitoa ushirikiano unaostahili hususani Idara ya Fedha na Kitengo cha TEHAMA ambao hushughulikia Mfumo wa Mapato uliounganishwa na TAMISEMI na Benki ya NMB kwa ajili ya Malipo ya Halmashauri
Awali akizungumza na Watumishi wa Benki ya NMB Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara ndugu Christopher Msimbe, aliwaeleza Watumishi hao kuwa Halmashauri yake inafurahia huduma za Benki ya NMB na kuongeza kuwa Benki hiyo imekuwa ni kichocheo cha ukuaji wa Uchumi katika Mji wa Ifakara kwa kutoa Mikopo kwa Wafanyakazi,Wafanyabiashara wadogo,wakati na wakubwa ambao wote hao kwa pamoja ndiyo Wanaolipa Ushuru na kodi mbalimbali za Serikali na kuiomba Benki hiyo kuwasiliana na Halmashauri yake mapema iwezekanavyo mara wanapobaini udanganyifu katika mikopo
Alipotakiwa kueleza kuhusu changamoto Kaimu Mkurugenzi alisema kuwa Halmashauri yake haijapata changamoto za kiutendaji na NMB hadi sasa bali umbali kati ya NMB na Halmashauri umekuwa ni changamoto kwa Wafanyabiashara wanaofanya malipo ya Halmashauri kupitia mfumo ambao umeunganishwa na NMB na kufafanua kuwa hilo si tatizo la NMB,hata hivyo Halmashauri inatafuta njia sahihi ya kushughulikia changamoto hiyo ili kuondoa usumbufu wa umbali kati ya Taasisi hizo mbili unaolalamikiwa na Wafanyabiashara na kuongeza Ufanisi wa Ukusanyaji Mapato ya Halmashauri
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa