Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Ndugu Francis Ndulane amewaongoza Wataalamu wake wa Idara ya fedha,biashara na masoko kutoa elimu ya kodi na ushuru kulingana na mabadiliko ya Sheria ya fedha za Serikali za Mitaa ya mwaka 2017 kwa Wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni mjini Ifakara.
Akizungumza na Wafanyabiashara hao hivi karibuni katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Ndulane amesema kuwa Menejimenti yake imeona ni vyema kukaa pamoja na Wafanyabiashara hao na kuelekezana mabadiliko ya msingi katika Sheria mpya ya fedha za Serikali za Mitaaa kulingana na Miongozo mipya iliyoletwa na Mamlaka za juu ambayo imeelekeza kufutwa au kupunguzwa kwa baadhi ya kodi zilizoonekana kuwa kero kwa Wananchi na kodi nyinginezo zimehamishiwa Serikali Kuu ambapo hapo awali zilikuwa zikikusanywa na Serikali za Mitaa na pia zipo kodi zinazoendelea kukusanywa na Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Miongozo mipya iliyotolewa.
“ Halmashauri ina jukumu kubwa la kutoa huduma kwa Wananchi lakini haiwezi kutoa huduma za msingi kama elimu na Afya ikiwa haina mapato ya kutosha na ikizingatiwa kuwa halmashauri bado ni changa hivyo tunahitaji kuikuza kwa kuwekeza katika kulipa kodi ndiyo maana tumewaita hapa kuwaelekeza kuhusu mabadiliko hayo ili muweze kulipa kodi bila shuruti”
Mkurugenzi alieleza kuwa Halmashauri imeweka mazingira mazuri kwa Wafanyabiashara wa nyumba za kulala Wageni kwa kuondoa ushuru kwa Wafanyabiashara wa Mpunga ambao ndiyo wateja wakubwa wa nyumba za kulala Wageni Ifakara kutokana na uwepo wa miundombinu yote muhimu kama viwanda vingi vya kukoboa Mpunga,umeme wa kuaminika, huduma za kibenki na usalama wa kutosha
Akitaja mabadiliko yaliyotokea katika Sheria hiyo ambayo yanawahusu Wafanyabiashara hao Mkurugenzi aliutaja Ushuru wa Hoteli ambao hapo awali ulikuwa ukitozwa kwa wenye nyumba za kulala Wageni ambao hawajaingizwa katika mfumo wa kodi ya ongezeko la thamani ‘VAT’ na wale waliokuwa katika VAT walikuwa wakitozwa ushuru wa huduma ambayo sasa umefutwa na Watu wote wenye nyumba za kulala Wageni watalipa Ushuru wa hoteli.
Naye Afisa Ushirika na Masoko wa Halmashauri hiyo Maliki Mabuba, alifafanua kuwa Sheria hiyo imegusa maeneo matatu ambayo ni ya Ushuru wa mazao,Ushuru wa Hoteli na faini zitakazotozwa kwa Watakaovunja Sheria hiyo ambapo alieleza kuwa Ushuru wa mazao ya biashara uliokuwa ukitozwa kati ya 3% - 5% na sasa utatozwa kwa 3% pekeee huku mazao ya chakula yakitozwa kwa 2% pekee.
Mabuba aliongeza kuwa Sheria hiyo inataka nyumba zote za kulala Wageni kulipiwa ushuru wa hoteli yaani ‘Hotel Levy” wakati huo huo ikifuta ushuru wa huduma “Service Levy” kwa nyumba zilizokuwa zikilipa Ushuru huo, hivyo Ushuru wa hoteli “Hotel Levy” utaendelea kutozwa na Halmashauri kwa mwaka huu wa fedha na hata kwa miaka ya nyuma kwa wale wote ambao hawakulipa, aidha aliongeza kuwa Sheria hiyo imefanya mabadiliko katika tozo ya faini kutoka kiwango kisichozidi Tsh.50,000/- na sasa ni kuanzia Tsh.200,000 hadi 1,000,000/- kwa watu wataokutwa na makosa ya Sheria hiyo ikiwemo ukwepaji kodi na kuongeza kuwa Ushuru wa mabango na kodi za majengo zitakusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania “TRA”
Katika majadiliano, Wafanyabiashara hao waliiomba Halmashauri kushusha kiwango cha Ushuru wa hoteli kutoka 10% hadi 5% ambapo pia walitaka tafsiri kuhusu tamko la Sheria linalotaka kulipa ‘Hotel Levy” kwa watu wanaomiliki nyumba za kawaida za kulala Wageni zinazoitwa “ Guest Houses” na “Lodges”
Akijibu hoja hizo Afisa biashara wa Mji, Baraka Munisi alisema kuwa Ushuru wa Hoteli ni takwa la Sheria Mama ya Fedha za Serikali za Mitaa hivyo kwa namna yeyote 10% haiwezi kupunguzwa hadi 5% bali asilimia hizo hutozwa kwa kiwango cha mapato ya Mfanya biashara hivyo kama atapata mapato makubwa atatozwa kiwango kikubwa ambacho ni 10% ya mapato yake na akipata kidogo atatozwa kiwango kidogo kwa 10% ya mapato yake, aidha kuhusu tafsiri ya Ushuru wa Hoteli alieleza kuwa nyumba zote zinazofanya biashara ya kulaza Wageni zitatozwa ushuru huo bila kujali hadhi ya nyumba hiyo wala aina ya jina lake.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa