Halmashauri ya Mji Ifakara imeng’ara katika matokeo ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa kushika nafasi ya 3 kati ya Halmashauri 9 za Mkoa wa Morogoro huku ikiwa ni mara yake ya kwanza kukimbiza Mwenge wa Uhuru kwa kujitegemea tangu Halmashauri ilipoanzishwa 2015.
Akiwasilisha salaam za pongezi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kilombero kwenye Mkutano wa Baraza maalum la Madiwani lililoketi hivi karibuni kutoa maoni katika rasimu ya Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Halmashauri, Katibu Tawala Wilaya ya Kilombero ndugu Robert Selasela aliwapongeza Wadau wote wa Halmashauri walioshiriki na kufanikisha Mbio za Mwenge wa Uhuru na kupelekea matokeo hayo mazuri
Katibu Tawala amesema kuwa hayo ni mafanikio makubwa sana kwa kuzingatia changamoto za uchanga wa Halmashauri na kusema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itaandaa kikao maalum kwa ajili ya kufanya tathmini na Wadau wote ili kuweza kujadili kwa pamoja changamoto zilizojitokeza na kuweka mikakati ya kufanya vizuri zaidi mwaka 2018.
Nao Watumishi wa Halmashauriya Mji Ifakara wameelezea kufurahishwa na matokeo hayo na kusema kuwa wanayo matarajio ya kufanya vizuri zaidi mwakani kwa kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka huu zimewapa ujuzi,kuwajengea uwezo na kuwapatia uzoefu wa kutosha wa kuratibu zoezi zima
“Ushirikiano na kujitoa kwa Watumishi na Wadau ndiyo kumeleta mafanikio hayo, hivyo mwakani tutaongeza juhudi na tutapata matokeo bora zaidi ya haya .Alisema Zuena Rapagani, Afisa Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mratibu Msaidizi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wa Halmashauri ya Mji.
Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Morogoro ulipita mwezi Juni 2017 na katika Halmashauri ya Mji Ifakara ulitembelea miradi 8 yenye jumla ya Tsh bilioni 1.6 wakati miradi 5 iliwekwa mawe ya msingi, miradi 2 ilizinduliwa na mradi 1 ulionwa.
Kilele cha Mbio hizo kitaifa kilifikiwa kisiwani Pemba Oktoba 14,mwaka huu ikiwa ni kumbukumbu ya kifo cha Muasisi na Baba wa Taifa Hayati Mwl.Julius Kambarage Nyerere na kupelekea hatua ya matokeo ya sasa ambapo kwa Mkoa wa Morogoro Halmashauri iliyoongoza ni Manispaa ya Morogoro, ikifuatiwa na Ulanga , Ifakara ,Kilombero, Malinyi , Morogoro DC ,Mvomero,Kilosa na Gairo ikiwa ni ya mwisho
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa