Halmashauri ya Mji Ifakara imetiliana saini mikataba ya Ujenzi wa Barabara zenye urefu wa Kilomita 108 kwa thamani ya Shilingi milioni 619 na Wakandarasi wa kampuni nne za kizalendo ikiwa ni kazi ya kwanza kwa kandarasi za ujenzi wa barabara tangu Halmashauri ya Mji Ifakara ianzishwe.
Akizungumza katika hafla ya uwekaji saini wa mikataba hiyo iliyofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero Mhandisi wa Ujenzi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Injinia Aristedes Soma amesema Ujenzi wa barabara hizo ni ukamilishwaji wa bajeti ya mfuko wa Barabara ya mwaka wa fedha 2016/17 na kwamba umegawanyika katika hatua nne ambapo awamu ya kwanza ni Ujenzi wa kawaida Kilomita 82,awamu ya pili ni matengenezo ya muda maalumu kilomita 11 na awamu ya tatu ni matengenezo ya sehemu korofi kilomita 15 na awamu ya nne ikiwa ni ujenzi wa madaraja na makaravati.
Injinia Soma ameongeza kuwa gharama za mikataba hiyo minne ni milionil 619 na kazi itaanza katika kipindi cha wiki moja tangu kutiliana saini kwa mikataba hiyo na kusisitiza kuwa kabla ya kufanya malipo Wahandisi wa Mji watafanya ukaguzi wa kina kukagua ubora wa kazi na Halmashauri haitolipa fedha yeyote ikiwa kazi iliyofanyika itakuwa chini ya kiwango kilichoainishwa katika mikataba.
Awali akifungua hafla ya Uwekaji saini mikataba hiyo iliyohudhuriwa na Viongozi na Watendaji wa Halmashauri, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mh.Mashaka Mbilinyi amesema kuwa Halmashauri inatarajia kazi nzuri ya ujenzi ,matumizi mazuri ya muda pamoja na ubora wa barabara na hivyo kuwaondolea adha ya miundombinu Wakazi wa Ifakara na kwamba Halmashauri haitarajii barabara kuharibika baada ya msimu mmoja .
“Sisi tutakuwa sambamba na Wataalamu wetu katika kaguzi za ujenzi na hatutokubali kupokea barabara zilizo chini ya kiwango hasa ikizingatiwa kuwa ninyi ndiyo Wakandarasi wa kwanza kujenga barabara za Mji wa Ifakara zingatieni Weledi na Utaalamu wenu ,fanyeni kazi nzuri ili muendelee kuaminika na kupatiwa kazi nyinginezo”.Alisema Mh.Mbilinyi.
Mwenyekiti huyo pia amewataka Wakandarasi hao kutoa kipaumbele cha ajira kwa vijana Wakaazi wa Mji wa Ifakara kwani vijana wapo wengi wenye sifa na hivyo kandarasi hizo ziwanufaishe Watu wa Ifakara na wao kama viongozi wapo tayari kutoa Ushiriakiano kwa Wakandarasi hao wakati wowote watakapohitajika.
Naye Eugine Moyo Mkurugenzi wa kampuni ya Cossiga CO.LT ya Jijini Dar es Salaam akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya zoezi la kutia saini mikataba kukamilika amesema wao watajitahidi kufanya inayolingana na thamani ya pesa kwa kufuata mikataba tena kwa wakati na kuushukuru Uongozi wa Halmashauri kwa kuwahakikishia ushirikiano na kuongeza kuwa Watafanya kazi yenye ubora hasa kwa kuwa uongozi umeshawaahidi kuwa fedha za ujenzi wa barabara hizo zipo tayari.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa