Ikiwa ni mwaka mmoja tu umetimia tangu Halmashauri ya Mji wa Ifakara kutangazwa na kukabidhiwa cheti rasmi cha kuanzishwa kwake,halmashauri hiyo imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya Tsh 45,000,000/ kwa vikundi 22 kati ya hivyo 17 vya Wanawake na 5 vya vijana toka katika kata nne za Mbasa,Viwanja Sitini,Ifakara na Mlabani .
Akitoa neno la utangulizi katika hafla fupi ya kukabidhi hundi hizo iliyofanyika siku ya maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania katika ukumbi wa Halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Francis Ndulane alisema fedha hizo zimetokana na makusanyo ya vyanzo vya ndani vya Halmashauri na kwamba vikundi hivyo ndiyo vya kwanza kupatiwa mikopo tangu halmashauri hiyo ianze kutekeleza majukumu yake yenyewe Julai 2015 na kwamba huo ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya kuwapatia mikopo Wanawake na vijana ili kuwawezesha katika shughuli za uzalishaji mali
Ndulane aliongeza kuwa upatikanaji wa vikundi hivyo vyenye watu zaidi ya 100 umekuwa shirikishi kwani mchakato wake umeanzia katika ngazi za vitongoji,mitaa na kuthibitishwa na mabaraza ya kata baada ya kukidhi masharti na vigezo vya kupatiwa mikopo ambayo ni usajili wa vikundi, kuwa na akaunti zilizo hai benki,vikundi kuwa ni vya vijana wasiozidi umri wa miaka 35 au wanawake,kuwa na shughuli maalumu na halali inayotambulika na kuwa na uzoefu wa shughuli waliyoombea mkopo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara Mashaka Mbilinyi aliwaomba wanufaika hao wa mikopo kuwa na nidhamu ya fedha hizo ili ziweze kuleta tija iliyokusudiwa na hatimaye wengine pia waweze kukopeshwa,aidha aliviomba vikundi hivyo kufufua magulio yaliyopo katika kata zao ili waweze kufanya biashara kwa uwanda mpana zaidi na kuiomba benki ya NMB kuendelea kuviimarisha vikundi hivyo katika shughuli zao za ujasiriamali na kuzalisha vikundi vingi zaidi ya hivyo.
Akihutubia kabla ya kukabidhi hundi za mikopo kwa vikundi hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo alisema Serikali itafuatilia fedha hizo hatua kwa hatua na kuwaagiza maafisa Maendeleo na maafisa Ushirika kutatua changamoto zitakazovikabili vikundi hivyo mara moja ili viweze kuzalisha na kurejesha fedha hiyo ndani ya muda uliokusudiwa.
“Fedha hizi sio za kwenda kufanyia Sherehe ya kumtoa Mwali,tutatoa muda wa kuzalisha na kuzifuatilia kwa karibu na atakayeshindwa kuzirejesha ataingia katika mgogoro wa kisheria na Serikali”.Alisisitiza Ihunyo.
Awali akizungumza na Waandishi wa habari, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Mji Ifakara Ally Ndyanabo alisema tayari Idara yake imevipatia vikundi vyote elimu ya Ujasiriamali,usimamizi wa fedha na uongozi wa vikundi ili kukabiliana na changamoto zitakazojitokeza ili kuviwezesha kufanya shughuli walizokusudia na kurejesha fedha hiyo kwa wakati.
Nao wanavikundi waliopatiwa mikopo hiyo waliishukuru Halmashauri kwa kuanza kuwapatia mikopo na mafunzo na kusema kuwa mafunzo waliyopewa yatawasaidia kuendesha shughuli zao kitaaamu tofauti na hapo awali walipokuwa wakijifanyia shughuli zao kienyeji na kwamba elimu waliyopatiwa wakati huu itawainua katika shughuli zao za ujasiriamali.
“Kulikuwa na changamoto ya uadilifu katika utunzaji wa fedha kabla ya kupata mafunzo,viongozi walikuwa wakifanya maamuzi ya fedha wao wenyewe wakati mwingine bila kutushirikisha lakini kwa sasa mambo hayo hayawezi kujitokeza tena kwa kuwa tumefundishwa uendeshaji wa vikundi na usimamizi wa fedha kwa pamoja”.Alisema Cleotida Claudi.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa