Ikiwa ni hatua ya kujidhatiti na kukabiliana na magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu ambacho tayari kimeripotiwa kuwepo wilaya jirani ya Kilosa,halmashauri ya Mji Ifakara imenunua mapipa ya taka 30 na kuyatawanya katika mitaa yake,pembezoni mwa barabara na maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu pamoja na kukarabati vizimba viwili.
Akizungumza na Wafanyabiashara wa soko kuu la Ifakara wakati wa uzinduzi wa vizimba na usimikaji wa mapipa hayo shughuli iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Francis Ndulane alisema kuwa Halmashauri imeona haja ya kukarabati haraka vizimba 2 vilivyogharimu Tsh 9,000,000/- kila kimoja kufuatia changamoto ya uchakavu wa kizimba kilichokuwepo sokoni hapo awali ambacho hakikukidhi mahitaji na kupelekea uchafu kuzagaa jambo lililohatarisha afya za Wafanyabiashara hao.
“Mtakumbuka kwa mara ya kwanza nilipotembelea soko hili mapema mwezi Oktoba mlinipa changamoto nyingi ikiwemo ya uchakavu wa kizimba,halmashauri imefanya juhudi ya kukikarabati na kukitanua kizimba hiki ili kiweze kuhifadhi taka zinazozalishwa sokoni hapa wakati wa mchana mpaka jioni Mkandarasi atakapokuja kuzibeba na kupeleka dampo,kwa uchache tumekarabati vizimba 2,kimoja ni hiki na kingine kipo stendi.”Alisema Ndulane
Aidha Mkurugenzi pia aliwaasa Wafanyabiashara hao kuendelea kulipa kodi na ushuru kwa wakati ili kuiwezesha Halmashauri kuboresha miundombinu ya masoko na mazingira ya wao kufanya biashara.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Ifakara Mashaka Mbilinyi aliwasihi Wafanyabiashara hao kukitumia kizimba hicho vizuri na kutoa taarifa mapema ikiwa Mkandandasi atachelewa kuchukua takataka katika kipindi cha masaa sita kilichokubalika katika Mkataba wa Mkandarasi huyo na kuwaomba kuwa Walinzi wa mradi huo kwa kuwa Wao ndiyo wanaojua hali halisi ya uchafu uliokuwa umekithiri katika soko hilo ambao kimsingi ulikuwa ni kero kubwa sana katika mazingira hayo ya biashara
Nao Wafanyabiashara hao waliishukuru Halmashauri ya Mji wa Ifakara kwa kuipatia ufumbuzi changamoto ya uchafu sokoni hapo na kuahidi kuwa Walinzi wa matumizi mazuri ya kizimba hicho na kwamba watahakikisha taka hizo zinaondolewa kwa wakati na ikiwa kutakuwa na changamoto wataziwasilisha ofisi ya Mkurugenzi mapema.
“Tunaishukuru sana Halmashauri kwa kusikia kilio chetu na tunaahidi tutasimamia uzoaji wa taka kwa wakati na ikiwa kutakuwa na kikwazo tutaripoti kwa wakati.”Alisema Hamisi Ruvu,Mwenyekiti wa umoja wa Wafanyabiashara sokoni hapo (UWASOKI).
Kizimba hicho kilizinduliwa na Mkuu wa wilaya ya Kilombero James Ihunyo baada ya kutoa maelekezo na kusisitiza utaratibu wa kuondosha taka hizo katika eneo hilo kwa wakati na kuendelea kuboresha mazingira ya usafi sokoni hapo.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa