BARAZA LA MADIWANI HALMASHAURI YA MJI WA IFAKARA
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Ifakara limeidhinisha kuanza mara moja ujenzi wa Ofisi za Halmashauri wa Mji huo baada ya kupata kibali toka kwa mwanasheria mkuu wa serikali.
Ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 7.4. Halmashauri ya mji wa Ifakara imeingia mkataba wa ujenzi na wakala wa majengo Tanzania (TBA) na kazi ya ujenzi wa Ofisi utachukua miezi 18.
Ofisi hiyo itajengwa katika eneo la Ofisi za serikali katika eneo la Bomani licha ya awali Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutoa ushauri kuwa Halmashauri kutafuta eneo lingine la ujenzi kutokana na eneo hilo kujaa Ofisi za serikali ikiwemo jengo la Halmashauri mama ya Wilaya ya Kilombero.
Hata hivyo Halmashauri baada ya kupokea barua ya ushauri kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imejadili ushauri huo na kuona haukuzingatia muda kwa maana mchakato wa ujenzi wa Ofisi kwa eneo la awali umeshafikia hatua za mwisho pamoja na kuridhiwa na vikao mbalimbali vya Halmashauri.
Pia kama Halmashauri wameona hawana eneo lingine kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi hizo za halmashauri ya mji wa Ifakara na eneo ambalo jengo la Ofisi litajengwa halihitaji fidia ya aina yeyote na pia eneo lililoteuliwa kwa ujenzi lipo katikati ya mji ambapo itarahisisha mawasiliano na Ofisi za umma na wananchi kwa ujumla.
Aidha, Halmashauri hiyo imesema wakala wa majengo nchini (TBA) ambapo ndiyo washauri wakuu wa ujenzi wa ofisi za serikali waliridhia ujenzi wa Ofisi katika eneo hilo na kubadilisha eneo la ujenzi wa Ofisi hizo ni kurudisha nyuma mchakato na kuiongezea gharama Halmashauri ambapo mpaka sasa imesha tumia shilingi milioni 36.7.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa