Baraza la Halmashauri ya mji Ifakara limepitisha makisio ya bajeti yenye jumla ya Tsh 22,717,294,506/- katika mwaka wa fedha 2017/2018 huku Tsh. 4,006,113,800 zikiwa ni vyanzo vya ndani pekee sawa 22.5% ya makisio ya bajeti nzima kwa mwaka wa fedha husika.
Akizungumza wakati wa Mkutano maalum wa Baraza la kujadili makisio ya bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa chuo cha Maendeleo kilichopo mjini Ifakara Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Francis Ndulane Ndulane alisema uhalisia wa makisio hayo utatokana na kuidhinishwa kwa Sheria ndogo za Halmashauri ambapo baadhi ya vyanzo vya ndani ili viweze kukusanywa vinahitaji mchakato wa Sheria ndogo kukamilika.
Alisema bajeti hiyo imejiwekea vipaumbe mbalimbali ikiwemo kuimarisha uwezo wa ukusanyaji wa mapato,kuhakikisha Biashara ndogo ndogo zinarasimishwa ili kujenga uwezo wa wafanyabiashara na kutangaza maeneo ya uwekezaji yaliyoainishwa kwenye ngazi ya kata na Halmashauri kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali,kuongeza kipato na kutoa ajira.
Aidha Halmashauri imejipanga kuhakikisha maeneo ya viwanja vya taasisi na sekta mbalimbali yanapimwa ili kuondokana na migogoro baina ya watumiaji,kuongeza tija katika kilimo na Mifugo na kuendelea kuboresha mazingira ya shule za msingi za wenye mahitaji Maalum.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alisema katika kufanikisha Mpango huo mapendekezo ya miradi yamezingatia miongozo ya kisekta ikiwemo uwepo wa ukomo wa rasilimali fedha ikilinganishwa na mahitaji,kutumia vigezo vya msingi wakati wa kuanzisha miradi na kumaliza miradi viporo badala ya kuanzisha miradi mipya.
Kuhusu ruzuku ya matumizi mengine na mishahara,Ndulane alisema Halmashauri inatarajia kupokea shilingi 16,473,937,106 kutoka Serikali kuu kama ruzuku ya matumizi ya kawaida na mishahara na kati ya kiasi hicho shilingi 1,701,337,106 itakuwa ni ruzuku ya matumizi ya kawaida na shilingi 14,772,600,000 ni ruzuku ya mishahara.
Kibaoni - Bomani
Sanduku la Barua: 433 Ifakara
Simu ya Mezani: +255 (0)23 - 2934212
Simu ya Mkononi: 0738 223 543
Barua Pepe: td@ifakaratc.go.tz / info@ifakaratc.go.tz
Haki Miliki @2018 Halmashauri ya Mji wa Ifakara . Haki zote zimehifadhiwa